9 KANEMBWA WATAKIWA KUWASILISHA UTETEZI

Release No. 020
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Februari 6, 2014

9 KANEMBWA WATAKIWA KUWASILISHA UTETEZI

Wachezaji tisa wa Kanembwa JKT pamoja na timu yao wanaolalamikiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kumpiga mwamuzi Peter Mujaya wanatakiwa kujitetea mbele ya Kamati ya Nidhamu itakayokutana Jumapili (Februari 9 mwaka huu).

Utetezi huo unaweza kuwa wa mdomo kwa walalamikiwa kufika wenyewe mbele ya kamati itakayokutana saa 4 kamili asubuhi au kuuwasilisha kwa njia ya maandishi.


Kamati ilikutana jana Jumatano (Februari 5 mwaka huu) kusikiliza malalamiko dhidi ya wachezaji hao na timu yao kwa tukio hilo lililotokea Novemba 2 mwaka jana kwenye mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) dhidi ya Stand United FC iliyochezwa Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Wachezaji hao ni Abdallah Mgonja, Bariki Abdul, Philipo Ndonde, Mbeke Mbeke, Mkuba Clement, Mrisho Mussa, Nteze Raymond, Ntilakigwa Hussein na Uhuru Mwambungu. Mlalamikiwa mwingine ambaye naye anatakiwa kujitetea ni timu ya Kanembwa JKT.

Ikiwa chini ya Mwenyekiti wake Tarimba Abbas, Kamati hiyo baada ya kusikiliza malalamiko dhidi ya wahusika na kupokea ushahidi wa aina mbalimbali kutoka kwa mlalamikaji imesema ili iweze kutenda haki katika shauri hilo ni lazima walalamikiwa wapate fursa ya kusikilizwa.

Katika hatua nyingine, Kamati hiyo iliyokutana kwa mara ya kwanza tangu ilipoundwa imesema imesikitishwa na vitendo vya fujo ndani ya mpira wa miguu, na kuwataka watu wasijihusishe na aina yoyote ya fujo.



EmoticonEmoticon